Umoja

Karudi baba mmoja, toka safari ya mbali,
Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili,
Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali,
Wakataka na kauli iwafe maishani.

Akatamka mgonjwa, ninaumwa
kwelikweli,
Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali,
Roho naona yachinwa, kifo kimenikabili,
Semeni niseme nini, kiwafae maishani.

Yakawatoka kinywani, maneno yenye akili,
Baba yetu wa thamani, sisi tunataka mali,
Urithi tunatamani, mali yetu ya halali,
Sema iko wapi mali, itufae maishani?

Baba aliye kufani akajibu lile swali
Ninakufa maskini baba yenu sina hali
Neno moja lishikeni kama mnataka mali
Kama mnataka mali mtayapata shambani

Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali
baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,
akili zetu nyembamba, hazijajua methali,
kama tunataka mali, tutapataje shambani?

Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,
fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,
haya sasa buriani, kifo kimeniwasili,
kama mnataka mali mtayapata shambani.

Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,
mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,
na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli,
kama mnataka mali, tutayapata shambani.

Fumbo wakatafakari, watoto wale
wawili.
Wakakata na shauri, baada ya siku mbili.
Wote wakawa tayari, pori nene kukabili.
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali.
Tangu zile za mibuni, hadi zitupazo wali.
Na mvua ikaja chini, wakaona na dalili.
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Shamba wakapalilia, bila kupata ajali.
Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali.
Wote wakashangilia, wakakumbuka kauli.
Kama mnataka mali, mtayapata shambani

Wakanunua na ng’ombe, majike kwa mafahali.
Wakapata na vikombe, mashine na baiskeli.
Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali.
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.

Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali.
Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali.
Wakakiweka kibao, wakaandika kauli.
“KAMA MNATAKA MALI MTAYAPATA
SHAMBANI”.

Advertisements

Its a pleasure reading your leave-in

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s